Kila 1 kati ya nchi 2 duniani hazipo tayari kuzuia na kutibu saratani: WHO

1 Februari 2013

Zaidi ya nusu ya nchi kote duniani hazina uwezo wa kuzuia na kutoa matibabu dhidi ya saratani, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani, WHO. Shirika hilo limesema nyingi ya nchi hizi hazina mpango tekelezi wa kudhibiti kansa, ambao unajumuisha kuzuia, kugundua mapema, kutibu na huduma za uuguzi.

WHO inasema kuna haja ya dharura kuzisaidia nchi hizi nyingi kupunguza vifo vitokanavyo na kansa, na kutoa huduma za matibabu na uuguzi kwa muda mrefu ili kuepusha maumivu ya wanadamu na kulinda maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi hizo.

Saratani ni mojawapo ya magonjwa yanayoongoza katika kusababisha vifo kote duniani. Zaidi ya thuluthi mbili za vifo hutokea katika nchi zinazoendelea. Dr. Andreas Ullich kutoka WHO anasema kansa vifo hivi vinaweza kuzuiliwa.

“Kila mwaka watu milioni 7.6 wanafariki dunia kutokana na saratani, huku takriban watu milioni 13 wakiwa wanapatikana na kansa kila mwaka. Ni mzigo mkubwa. Lakini kuna matumaini, tnajua kuwa, hadi thuluthi moja ya vifo vitokanavyo na kansa vinaweza kuzuiliwa kwa kuepuka, vitu vinavyoweza kuisababisha, vikiwemo matumizi ya bidhaa za tumbaku, unene wa kupindukia, matumizi ya pombe, kutofanya mazoezi na magonjwa ya kuambukiza katika baadhi ya maeneo ya dunia, ambayo yanaweza kuzuiliwa kwa chanjo”

WHO inasema, ili kupunguza hatari za vitu vinavyosababisha kansa na kuhakikisha kila mtu aliye na kansa anapata matibabu, programu za kina za kudhibiti kansa zinatakiwa kuwekwa katika kila nchi.