Uendeshaji wa kesi ya ubakaji Somalia inatia wasiwasi: UNPOS

1 Februari 2013

Kuhusu maswala ya haki nchini Somalia, Afisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kisiasa nchini Somalia (UNPOS), imeelezea wasiwasi wake kuhusu jinsi kesi inayohusu madai ya ubakaji dhidi ya mwanamke mmoja wa Kisomali inavyoendeshwa.

Watu watano wameshtakiwa katika kesi hiyo iliyofunguliwa na polisi ikisema kuwa habari zilizochapishwa kuhusu madai ya ubakaji huo, zilikuwa za uwongo. Mwandishi habari Abdiaziz Abdinur Ibrahim ameshtakiwa kwa madai ya kudhalilisha hadhi ya taasisi ya kitaifa, huku watu wengine wanne, akiwemo mwanamke aliyedaiwa kubakwa, wakishtakiwa kuhusiana na kesi hiyo, ambayo inatarajiwa kuanza kesho Februari 2 kwenye mahakama moja mjini Mogadishu.

UNPOS imeelezea wasiwasi wake kuhusu kuzuiliwa kwa muda mrefu kwa washukiwa, pamoja na kutowaruhusu kuzungumza na wakili mwanzoni- hali ambayo sasa imerekebishwa. UNPOS imesema hali hiyo inaathiri vibaya utekelezaji wa haki, na kwamba inatarajia kesi hiyo itaendeshwa kwa misingi ya sheria za kitaifa na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud