Hali ya kibinadamu nchini Somalia yaimarika

1 Februari 2013

Kaimu mratibu wa Umoja wa Mataifa juu ya shughuli za misaada ya kibinadamu nchini Somalia Stefano Porretti, amepongeza maendeleo makubwa yaliyofikiwa nchini humo na kusifia kitendo cha kuwakwamua wananchi waliotumbukia kwenye mzozo ambao sasa wamepungua hadi kufikia milioni 1.05.

Hata hivyo afisa huyo ameonya kuwa mafanikio hayo yanaweza kuporomoka kama kutakosekana mipango endelevu. Amesema tangazo la kupungua idadi ya watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu inatoa picha jinsi mbinu za ubunifu zilivyoweza kufanya kazi lakini kikubwa zaidi ni msimu mzuri wa mvua ulioshuhudiwa katika eneo hilo.

Taarifa zaidi na George Njogopa.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amekaribisha na kupongeza  maendeleo hayo yaliyofikiwa lakini ameonya kuwa hali ya misaada ya kibinadamu nchini Somalia inasalia kuwa tete akisema zaidi ya watu milioni moja bado wako kwenye mahitajio.

Amesema kuwa idadi hiyo ya watu bado inaandamwa na hali ngumu ya maisha, ikishindwa kupata mahitaji muhimu ya kila siku.

Bwana  Porretti  amesema kiasi kingine cha watu milioni 1.7 waliotoka kwenye machafuko katika kipindi cha miaka iliyopita, nao wanakabiliwa na kitisho cha ukosefu wa chakula na kuonya kuwa hali hiyo kama itaendelea kupuzwa inaweza kulizamisha taifa hilo kwenye hali ngumu zaidi.

Mpango uliolenga kuikwamua Somalia ulianzishwa Disemba mwaka jana ukiwa na lengo la kuinua ustawi wa taifa hilo na kushughulikia vipaumbele vya taifa. Katika kipindi cha mwaka huu pekee, kunahitajika kiasi cha dola za kimarekani biliono 1.3 ili kuupa msukumo mpango huo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter