Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ijue Radio ya Umoja wa Mataifa

Ijue Radio ya Umoja wa Mataifa

Radio ya Umoja wa Mataifa imetoka mbali, kuanzia mwaka 1946 ilipoanzishwa katika ofisi na studio za kuhama hama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Hapo ndio ilianza kurusha matangazo yake ya kwanza kabisa yakisema “Huu ni Umoja wa Mataifa ikiwaita wakazi wote wa dunia.” Vipindi kama vile taarifa za habari na makala vilitangazwa kwa lugha tano rasmi za kwanza za Umoja wa Mataifa ambazo ni Kichina, Kiingereza, Kifaransa, Kirusi na Kihispania kwa muda wa kati ya saa Tisa na saa 12 kwa siku. Lugha ya Kiarabu iliongezwa na kuwa rasmi mwaka 1974.

Kutokana na kukosa vifaa vyake yenyewe huku ikiwa imeaminiwa kwa kupatiwa taarifa muhimu za kuweka ajenda maalum baada ya vita vikuu vya pili vya dunia juu ya amani na ulinzi wa kimataifa, Radio ya Umoja wa Mataifa ilifanya mpango na mashirika makubwa ya utangazaji ili iweze kurusha vipindi vyake katika maeneo mbali mbali duniani. Mwaka 1964, kitengo cha matangazo ya kimataifa cha Wizara ya mambo ya nje ya Marekani kilirusha duniani kote matangazo yote ya Baraza la Usalama na yale ya Baraza la Uchumi na kijamii, ECOSOC kwa masafa mafupi. Matangazo hayo yalirushwa pia kwa kiasi kikubwa na Idara ya Ulaya ya Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC.

Kuanzia mwaka 1950 hadi 1959 radio ya Umoja wa Mataifa ilirusha matangazo yake ya saa Sita kwa lugha 33 kwani nchi 100 na maeneo zilikuwa zikipokea na kutangaza tena matangazo hayo kwa lugha zao wenyewe. Katika kipindi cha kati ya mwaka 1960 hadi 1979, vipindi vya Radio ya Umoja wa Mataifa vilijumuisha; mikutano kutoka makao makuu ya Umoja wa Mataifa iliyorushwa katika masafa mafupi, mikutano ambayo ilikuwa inafuatiliwa au kupokelewa na kutangazwa upya na mashirika ya utangazaji ya kitaifa. Halikadhalika matangazo ya masafa mafupi ya taarifa za habari katika lugha sita rasmi za Umoja huo, habari kwa ufupi na hata makala katika lugha 33 kufikia nchi 162 na maeneo zilizokuwa zikipokea matangazo hayo na kutangaza kwa lugha zao.

Radio ya Umoja wa Mataifa ilitumia mitambo ya kurushia matangazo iliyokodi kutoka Ufaransa, Uswisi, Italia na Marekani. Mwaka 1963, kulipatikana vifaa na mitambo ya kurushia matangazo yenye nguvu zaidi na uwezo wa kufika hadi Afrika, Ulaya, Amerika kusini, Mashariki ya Kati na baadhi ya maeneo ya Kusini Mashariki mwa Asia.

Mwaka 1984 Radio ya Umoja wa Mataifa ilikuwa ikiandaa vipindi vya jumla ya saa Elfu Mbili kwa mwaka katika lugha 25 ikihudumia nchi 167 na maeneo. Vipindi vyake vilivyorushwa katika masafa mafupi vilikuwa na jumla ya saa 759 kwa mwaka. Mwishoni mwa mwaka 1985, matangazo kupitia masafa mafupi yalisitishwa kutokana na kupanda kwa gharama za mitambo ya kurushia matangazo. Mbinu mbadala za kusambaza vipindi zilitafutwa na kubainika ambapo watangazaji wadau walipatikana barani Afrika, Amerika Kusini na Karibian,

Lugha za matangazo ya Radio ya Umoja wa Mataifa sasa ziko Nane ambapo zilizoongezeka ni Kiswahili na Kireno. Radio ya Umoja wa Mataifa imepata umaarufu zaidi katika operesheni za ulinzi wa amani. Uwezo wa radio kufikia watu wengi na kwa gharama nafuu umefanya Radio ya Umoja wa Mataifa kuwa na dhima kubwa katika operesheni hizo duniani kote. Katika operesheni zote hizo za ulinzi wa amani, Radio ya Umoja wa Mataifa hutoa wafanyakazi na vipindi na usaidizi wa kiufundi. Ripoti kutoka maeneo husika, habari na makala kuhusu ulinzi wa amani na usaidizi wa kibinadamu vimekuwa vikifanyika.

Na hii ndio Radio ya Umoja wa Mataifa!