Jiunge na Umoja wa Mataifa

4 Februari 2013

Umoja wa Mataifa, kimbilio la ulimwengu wakati wa matatizo magumu duniani kote: Kuanzia kumaliza migogoro, kuondoa umaskini, kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, na utetezi wa haki za binadamu. Masuala ndani ya ajenda za Umoja wa Mataifa ni mengi na tofauti kama vile ilivyo kwa fursa za ajira zinazotolewa na umoja huo.

Miongoni mwa wafanyakazi wapo wanaofuatilia chaguzi, wanaopokonya silaha askari watoto, wanaoratibu misaada ya kibinadamu kwenye mizozo na kutoa misaada ya shughuli za kiutawala au kusafirisha vifaa wakati Umoja wa Mataifa unapokuwa unatekeleza wajibu wake sehemu mbali mbali duniani. Hiyo ni baadhi tu ya mifano ya majukumu yanayofanywa na Umoja wa Mataifa.

Wigo mpana wa majukumu una maana kwamba ukiwa mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa unaweza kubadili majukumu, idara, eneo la kufanyia kazi na hata shirika wakati wote wa ajira yako ndani ya Umoja wa Mataifa.

Kuna wafanyakazi takribani Elfu Arobaini na Wanne kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa. Ikimaanisha kwamba utajikuta unafanya kazi na timu ya watu wenye tamaduni mbali mbali na historia tofauti za maisha, walio na uzoefu, matarajio na mifumo tofauti ya utendaji kazi. Umoja wa Mataifa huajiri watu kwa ajili ya operesheni za kulinda na kuleta amani, misaada ya kibinadamu, katika ofisi zake zilizosambaa maeneo mbali mbali duniani kama vile Geneva, Nairobi, Kabul, Dili, Addis Ababa, Kinshasa, Pristina, Bangkog hadi New York, hizo zikiwa ni ofisi chache tu kati ya nyingi zilizopo.

Je umepata motisha wa kujiunga? Je unajituma katika kazi na uko tayari kujitoa kwa lengo kuu la kusaidia binadamu? Na je matumaini na uwezo ni mambo ambayo yataongoza ari yako ya kuleta mabadiliko ndani ya dunia hii iliyosheheni mambo magumu? Je wewe ni mtu ambaye yuko tayari kusafiri na kufanya kazi pahali popote pale pindi anapotakiwa kufanya hivyo? Je unaweza kuchomoza katika mazingira ambayo kwa dhati ni ya kimataifa na tamaduni mbali mbali ambayo yanaheshimu na kuendeleza tofauti mbali mbali kwa kiasi kikubwa kwa kutumia jitihada za pamoja za watu mbali mbali?

Hizo ni baadhi tu ya sifa za wafanyakazi wetu. Umoja wa Mataifa unataka watu ambao wana maadili, wanajali usawa, hawana upendeleo, waaminifu na wakweli.

Umoja wa Mataifa unataka mtu anayekwenda na mabadiliko, ambaye haogopi kuwa na fikra za kibunifu, anajituma na anachukua hatua jambo linapotokea.

Iwapo unadhani una sifa hizo basi Umoja wa Mataifa ni sehemu yako ya kufanya kazi.

Ili kufahamu zaidi kuhusu ajira ndani ya Umoja wa Mataifa na jinsi ya kuomba nafasi za kazi kwa kada zote tembelea tovuti yetu Careers.un.org