Feltman azungumzia uchaguzi mkuu wa Kenya 2013-01-31

31 Januari 2013

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa ambaye pia ni msimamizi  mkuu wa masuala ya siasa ndani ya Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman amekuwa na mazungumzo na viongozi nchini Kenya ambapo ametaka uchaguzi mkuu wa nchi hiyo mwezi Machi mwaka huu ufanyike kwa uwazi na kwa amani.

Feltman ambaye amekutana na viongozi wa tume huru ya uchaguzi ya Kenya amesema uchaguzi huo utafuatiliwa kwa karibu ulimwenguni kote na kwamba anatumia fursa hiyo kuwasihi wakenya watekeleze haki yao hiyo ya kimsingi ya kidemokrasia kwa amani na utulivu.

Akizungumza mjini Nairobi, Kenya amesifu maandalizi yaliyofanywa na tume hiyo ikiwemo kuandikisha wapiga kura kwa wakati na harakati zinazoendelea za kuepusha ghasia.

Halikadhalika amegusia pia jukumu la viongozi wote akiwataka wazingatie sheria huku wakiwapatia wafuasi wao ujumbe thabiti kuwa ghasia ya aina yoyote haitakubalika.

Uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 nchini Kenya ulifuatiwa na ghasia ambapo watu zaidi ya Elfu Moja waliuawa na wengine 3,500 kujeruhiwa huku Laki sita wakipoteza makazi yao.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter