UNHCR yasifu mchango wa wahisani wa dola Bilioni 1.5 kwa Syria

31 Januari 2013

Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, António Guterres amesifu nchi wahisani kwa mchango wao wa zaidi ya dola Bilioni Moja na Nusu kusidia raia wa Syria waliojikuta katika maisha ya ukimbizi baada ya mgogoro kukumba nchi yao.

Amesema mchango huo uliotokana na mkutano wa Kuwait ni wa kipekee na utawawezesha kutoa msaada zaidi kwa wananchi wa Syria ambao wanakumbwa na madhila ikiwemo ukosefu wa malazi, chakula, dawa na hata huduma nyingine muhimu za kijamii.

Halikadhalika Guterres ametaka msaada zaidi pia kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi wa Syria ikiwemo Jordan, Uturuki, Lebanon na Iraq.

Hata hivyo haikufahamika mara moja mgao wa UNHCR katika fungu hilo jipya kwa kuwa shirika hilo nalo limekuwa likiomba msaada zaidi wa fedha ili kuwezesha kazi zake za kusaidia wakimbizi wa Syria.

Hadi Jumatano, UNHCR ilikuwa imepokea asilimia 22 tu ya fedha inazohitaji ikiwe ni ahadi na fedha taslimu kwa ajili ya operesheni zake huko Syria.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter