Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Lebanon Derek Plumbly leo ametembelea kambi ya Ain El-Hilweh kusini mwa Lebanon ambapo amejionea mazingira magumu ambamo wanaishi wakimbizi wakiwemo wale wa kipalestina waliokimbia mgogoro Syria.
Katika ziara hiyo ambapo Bwana Plumbly aliambatana na Ann Dismor, Mkurugenzi wa UNRWA nchini Lebanon, ameshuhudia vile ambavyo wanawake na watoto wanavyoishi kwenye hali ngumu na kusema inasikitisha.
Hata hivyo amesifu vile ambavyo UNRWA inatumia rasilimali ilizonazo kusaidia wakimbizi hao ambapo pia alikutana na wawakilishi wa vikundi mbali mbali ikiwemo vya wanawake na vijana kwenye kambi hiyo na kupongeza jitihada zao za kuboresha maisha licha ya mazingira magumu.
Kambi hiyo inahifadhi zaidi ya wakimbizi Elfu 55 wa kipalestina wakiwemo Elfu Nne waliokimbia Syria.