Tumejizatiti kuisaidia Somalia: UM

31 Januari 2013

Umoja wa Mataifa umejizatiti kusaidia Somalia kujenga amani ya kudumu, na hiyo ni kauli ya Mkuu wa masuala ya siasa ndani ya Umoja wa Mataifa Jeffery Feltman ambayo aliitoa mara baada ya mazungumzo yake na vinogozi wa nchi hiyo mjini Mogadishu.

Feltman licha ya kuonyesha wasiwasi wake juu ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo ukatili wa kingono dhidi ya wanawake, amesema anaridhishwa na jitihada za serikali za kujenga amani na ameitaka serikali kuendeleza mashauriano ya kitaifa.

(SAUTI YA FELTMAN)

Tunafahamu fika kuwa hatma ya Somalia iko mikononi mwa wasomali wenyewe na kwamba maamuzi kuhusu hatma ya Somalia iko mikononi mwa viongozi wa Somlia na wananchi wake na sisi tuko hapa kusaidia mchakato huu wa Somalia.”

Akiwa Somalia alikuwa na mazungumzo na viongozi mbali mbali akiwemo Waziri Mkuu Abdi Farah Shirdon, ambaye ameelezea kuridhishwa na mazungumzo ambayo amesema yalijikita katika msaada wa Jumuiya ya Kimataifa kwa Somalia.

(SAUTI YA SHIRDON)

Nimefurahishwa na mambo niliyojadili naye na tumekubaliana. Hii inaonyesha jinsi ambayo dunia inajihusisha na Somalia mpya na vile ambavyo inasikilia na kujiweka tayari kusaidia. Tunaunga mkono hatua hizo na tunafurahishwa nazo.”

Somalia imeshuhudia mabadiliko makubwa ambapo mwezi Septemba mwaka jana serikali ya mpito iliyodumu kwa miaka minane ilihitimishwa kwa uchaguzi wa Rais mpya kwenye mchakato ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter