Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Brahimi ataja vikwazo vya utatuzi wa mgogoro wa Syria

Brahimi ataja vikwazo vya utatuzi wa mgogoro wa Syria

Mjumbe maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za kiarabu katika mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi amesema kitendo cha pande mbili kwenye mzozo huo kutozungumza kabisa kinafanya utatuzi kuwa mgumu.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Radio ya Umoja wa Mataifa, mjini New York, Marekani, Brahimi amesema kila upande ina mtazamo wake juu ya chanzo cha mzozo huo ambapo serikali inaamini kuna nguvu za kigeni hivyo ni lazima ilinde eneo lake na wapinzani wanaamini ni utawala mbovu hivyo ni lazima wakabiliane nao.

Brahimi amesema bado nyaraka ya Geneva ina nafasi kubwa ya kutatua mzozo huo lakini kwanza anashauriana na nchi zenye ujumbe wa kudumu kwenye baraza la usalama ili kupata tafsiri sahihi ya nyaraka hiyo hususan chombo cha usimamizi wa kipindi cha mpito nchini Syria.

(SAUTI YA BRAHIMI)

“Kile ambacho nimekuwa najaribu kufanya ni kuona kama wajumbe watano wa kudumu kwa kuanzia na Urusi na Marekani zinaweza kukubaliana na kuwa na uelewa mmoja kuhusu nyaraka ya Geneva na tuichukue kama makubaliano ya kimataifa au azimio la baraza la usalama ili litekelezwa kupitia mashauriano ya pande hizo mbili.”

Kuhusu madai ya watu wengine kuwa suluhisho la kijeshi ni bora kuliko mashauriano ya mezani, Bwana Brahimi ametetea msimamo wake wa suluhisho kwa mazungumzo.

(SAUTI BRAHIMI)

“Unaweza kusema wako sahihi, hadi sasa jitihada za kufanya mashauriano hazijawa na mafanikio. Halikadhalika nguvu za kijeshi pia hazijaweza kumaliza mzozo. Tena nguvu za kijeshi zimekuwa na madhara makubwa kwa wananchi na nchi nzima. Kama tunaweza kuanzisha mashauriano kwa sasa, hamna anayesema ni rahisi lakini ni vyema zaidi kuliko kuuana,”.