Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO kuisaidia Mali kukarabati na kuokoa maeneo ya urithi wa dunia

UNESCO kuisaidia Mali kukarabati na kuokoa maeneo ya urithi wa dunia

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Irina Bokova, ametangaza kuwa shirika hilo litaisaidia nchi ya Mali kukarabati na kurejesha maeneo yake ya urithi wa kiasili, ambayo ameyataja kuwa sehemu muhimu ya historia na utamaduni wa nchi hiyo. Bi Bokova ametoa wito kwa wadau wote wa UNESCO kuunga mkono juhudi za ukarabati huo kama suala la kipaumbele.

Ameelezea pia kusikitishwa kwake na uharibifu wa maeneo hayo ya urithi wa dunia ambao ulishuhudiwa hivi karibuni, na kusema kuwa UNESCO itafanya kila iwezalo kushirikiana na watu wa Mali kukomboa urithi wao huo wa asili.

Maeneo ambayo yanatarajiwa kukarabatiwa ni pamoja na makaburi ya kihistoria mjini Timbuktu, na kaburi la Askia, Gao. Bi Bokova amesema kazi ya ujenzi itaanza mara tu hali ya usalama itakapoimarika.

Ametoa wito kwa viongozi wa nchi jirani za Mali, mtandao wa polisi wa kimataifa, Interpol pamoja na watu wanaohusika katika biashara za sanaa kufanya kila wawezalo kuzuia biashara haramu za bidhaa za urithi wa asili kutoka Mali.