Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watu Ulaya wanakata tamaa kufuatia mdororo wa kiuchumi: IFRC

Mamilioni ya watu Ulaya wanakata tamaa kufuatia mdororo wa kiuchumi: IFRC

Wakati bara la Ulaya likiwa bado linakumbwa na mdororo wa kiuchumi, Shirikisho la mashirika ya Msalaba Mwekundu na Mwezi Mwekundu (IFRC) limeonya kuwa mamilioni ya watu ambao wameathiriwa na ukosefu wa ajira, ongezeko la umaskini, kupoteza makazi na hali ya sintofahamu kuhusu hatma yao huenda wakakata tamaa.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni zaidi za jumuiya ya nchi za Ulaya (EU), zaidi ya watu milioni 26 katika mataifa 27 ya EU na kwingineko Ulaya na Asia ya Kati hawana ajira. Mashirika ya Msalaba Mwekundu na Mwezi Mwekundu yanaripoti kuwa idadi ya watu wanaokwenda kuomba misaada kutoka kwao imeongezeka. Anita Underlin ni Mkurugenzi kutoka IFRC kanda ya Ulaya.

(SAUTI YA ANITA)

Kwa sasa kuna ongezeko la idadi ya watu wanaokwenda Msalaba mwekundu kuomba msaada. Yapo yale makundi ya kawaida ambayo yako hatarini kila wakati. Lakini sasa kuna watu wapya ambao wanakuja, tunasema ni kundi jipya la maskini, watu ambao katika maisha yao hawajawahi kabisa kuomba msaada, lakini sasa wanajikuta katika mazingira ambayo lazima waende msalaba mwekundu au mwezi mwekundu kuomba msaada.”

Nchi za Uhispania na Ugiriki, ambazo ndizo zilizoathiriwa zaidi na mdororo wa uchumi, zina idadi kubwa zaidi ya watu wasio na ajira.