Skip to main content

Ukata wa bajeti usikwamishe mchango kwa Syria: Ban

Ukata wa bajeti usikwamishe mchango kwa Syria: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezungumza katika mkutano wa wahisani kwa ajili ya Syria huko Kuwait na kusema kuwa mazingira magumu yanayokumba wasyria hayawezi kuachwa yaendelee licha ya kwamba serikali mbali mbali duniani zinakumbwa na ukata.

Amesema anatambua hali ngumu ya uchumi lakini ombi la dharura la dola Bilioni Moja na Nusu kwa ajili ya miezi sita ijayo kuwahudumia wakimbizi wa Syria walio ndani na nje ya nchi yao ni muhimu likasikilizwa.

Bwana Ban amesema wanawake na watoto wa Syria wanakumbwa na hali ngumu ya kibinadamu, maisha ya kuhamahama baridi kali huku mapigano yakiwa yanaendelea na watoto wanataka kwenda shule huku zaidi ya watu Elfu Sitini wakiwa wamepoteza maisha.

(SAUTI YA BAN)

 “Tunahitaji msaada wenu. Ninatambua fika mashinikizo ya bajeti yanayokabili serikali wakati huu. Lakini hatuwezi kukubali ukata utuzuie kuwapatia misaada ya uokozi watu walio katika mahitaji makubwa. Bila rasilimali hatuwezi kutekeleza wajibu. Bila rasilimali watu wengi zaidi watakufa. Udharura huu unahitaji jitihada za hali ya juu zaidi. Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, watu binafsi, sekta binafsi, wote wana jukumu la kutekeleza.”

 Tayari Kuwait imetangaza mchango wa dola Milioni 300 ambapo Bwana Ban ameongeza kuwa umwagaji damu nchini Syria utamalizwa pindi kutakapokuwepo na suluhisho la kisiasa la mgogoro huo.

Kando ya mkutano huo Bwana Ban amekuwa na mazungumzo na viongozi wa Kuwait, Jordan, Uturuki na Bahrain.