Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajawazito waona mwanga Somalia

Wajawazito waona mwanga Somalia

Taifa la Somalia linazidi kuimarika kila uchwao baada ya kuundwa kwa serikali mwaka jana. Huduma za kijamii ikiwemo za kiafya zinazidi kuimarika. Hii imewezesha hata wajawazito ambao awali walikuwa wanajifungulia majumbani, kupata huduma hizo kwenye hospitali chini ya uangalizi wa madaktari, wauguzi na wakunga wenye uzoefu an vifaa.

Kitendo hiki kinaokoa siyo tu maisha ya mtoto bali pia ya mama na hivyo kusaidia utekelezaji wa malengo ya milenia ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga. Je nini kimefanyika huko Somalia? Tujiunge na Alice Kariuki kwa ripoti kamili.

Kwa miongo kadhaa sasa, maisha nchini Somalia yamekuwa ni ya kuhangaikia ili kuweza kuishi: kuhangaika kutokana na vita, njaa na ghasia. Mgogoro ambao nchi hiyo imeshuhudia, umemgusa kila mtu na zaidi kabisa ni wanawake. Wiki chache zilizopita, Guduudo Galinle mmoja wa wanawake waliopoteza makazi, alijifungua mtoto wake wa tano, mtoto wa kike ambaye amempatia jina la Fartum. Watoto wake wengine wote alijifungulia nyumbani, lakini huyu alilazimika kwenda hospitali kwani maisha ya mama na mtoto yalikuwa hatarini.

Hivyo basi Guduudo alikimbizwa kituo cha tiba cha Galkayo.

SOUNDBITE (Somali) Guduudo Galinle,

"Mahali pazuri zaidi pa kujifungulia ni hospitalini kwa sababu unapata msaada iwapo jambo lolote linatokea. Huwa najifungulia nyumbani wakati mwingine kwa sababu nakuwa siko tayari lakini kwa kawaida ni salama zaidi kwenda hospitali.”

Kituo cha tiba cha Galkayo kilianzishwa na Dokta Abdulakadir Giama mwaka 1997. Awali kituo hicho kilikuwa cha kibinafsi kikitoa zaidi huduma kwa wazazi. Hata hivyo kutokana na ongezeko la mahitaji kilibadilika na kwama 2005 kilifungua milango yake kwa watu waliopoteza makazi kutoka maeneo yote ya Galkayo. Dkt Giama ni Mganga Mkuu wa kituo hicho

SOUNDBITE (English) Dr. Abdulkadir Giama, Chief Doctor, Galkayo Medical Centre (GMC):

"Tunalazimika kutoa huduma kwa wanawake wakati wa ujauzito na kuhakikisha wanapata huduma nzuri kabla ya kujifungua. Hii inawezesha kufahamu iwapo kuna hatari yoyote kwa mzazi. Tunafuatilia wakati wa ujauzito, wakati wa uchungu na hata baada ya kujifungua.”

Misaada ya wahisani hususan kutoka nchi za Falme za kiarabu zimewezesha kituo hicho kupata vifaa vya kisasa kama vile maabara, x-Ray, kliniki zinazohamahama . kwa sasa kituo hicho kimebadilika na kuwa hospitali ya Rufaa kwa Somalia.

Misaada hiyo imewezesha kituo kupanua huduma zake. Saruuro Robow Ishak amekuwa mkunga kwa zaidi ya miaka Kumi. Amejifunza mwenyewe kazi hiyo. Lakini hivi karibuni alipata mafunzo ya uzazi salama.

SOUNDBITE (Somali) Sarruro Robow Ishak, Midwife:

"Hatari ambazo alikuwa anakabiliana nazo mjamzito ilikuwa ni kubwa zaidi na hatukuwa na ujuzi wa kutosha na vifaa. Awali tulikuwa tunatumia tu nyembe lakini hospitali hii imetupatia mafunzo na kikasha kizima chenye vifaa salama vya uzazi ikiwemo karatasi la nailoni na sababu ya kutumia ili kuondoa vimelea.”

Kwa Dokta Giama, msaada ambao kituo chake kimepokea umekuwa ni muhimu sana. Guduudo na Fartum sasa wamerejea nyumbani ikiwa ni ushahidi tosha kuwa upatikanaji wa huduma salama za tiba ambazo awali zilikuwa ni adimu kwa sasa zinaokoa maisha yao.

Nuru imeingia Somali na bila shaka malengo ya Milenia yako mbioni kufikiwa. Asante Alice kwa ripoti hiyo na kwako msikilizaji kwa kujumuika nasi. Basi hadi wakati mwingine kwa ripoti nyingine mimi ni Monica Morara, kwaheri kwa sasa.