Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa WHO afariki dunia

28 Januari 2013

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni WHO Dkt. Hiroshi Nakajima amefariki dunia nchini Ufaransa baada ya kuugua kwa muda mfupi.Alikuwa na umri wa miaka 84.

Taarifa za kifo hicho zimetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa sasa wa WHO Dr. Margaret Chan ambaye amemwelezea Nakajima kama mtu aliyojitoa kwa dhati na kulitumikia shirika hilo kwa uwezo wake wote.

Baadhi ya mambo ambayo Nakajima alikuwa mstari wa mbele kuyapigania ni pamoja uanzishwaji wa program ya kukabiliana na ugonjwa wa kifua kikuu iliyoanza kutekelezwa mnamo mwaka 1995 na mpango wa chanjo kwa watoto wote.

Dkt. Nakajima alijiunga na WHO mnamo mwaka 1974 na kuanzia mwaka 1988 hadi 1998 alishika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo.Ameacha mjane na watoto wawili.