Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu Syria yazidi kudorora

Hali ya kibinadamu Syria yazidi kudorora

Umoja wa Mataifa unasema hali ya kibinadamu nchini Syria inazidi kudorora kila uchwao ambapo watu Milioni Nne wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Shirika la kuratibu masuala ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA linasema baridi kali imeongeza madhila ya watu hususan wale waliohama makwao kutokana na mgogoro unaoendelea nchini mwao na sasa wanaishi kwenye makazi ya muda.

Watu hao hawana vifaa vya kuwawezesha kuweka mazingira ya joto ikiwemo nguo na mablanketi ambapo ukosefu wa mafuta unakwamisha uwezekano wa kutumia umeme kuzalisha joto.

OCHA inasema uhaba huo wa mafuta ikiwemo dizeli umekuwa kikwazo kikubwa cha usambazaji wa vifaa.