Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia, DRC, Madagascar, Zimbabwe zamulikwa huko Addis Ababa

Somalia, DRC, Madagascar, Zimbabwe zamulikwa huko Addis Ababa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa na mazungumzo na viongozi wa Afrika ambapo wamefanya mashauriano kuhusu masuala kadhaa ikiwemo yua kiuchumi, kisiasa na kijamii. Taarifa zaidi na Alice Kariuki.

Miongoni mwa viongozi aliokutana nao Bwana Ban ni Paul Kagame wa Rwanda ambapo wamejadili hali ya usalama katika nchi za Maziwa Makuu na amepongeza Rwanda kwa kupata ujumbe usio wa kudumu katika Barza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2013 na 2014.

Katika mazungumzo yake na Rais Joseph Kabila wa DRC, Bwana Ban amemsifu kiongozi huyo kwa utayari wake wa kupatia suluhu ya kudumu mgogoro Mashariki mwa nchi yake na kusema Umoja wa Mataifa umejizatiti kushirikiana kumaliza changamoto zilizobakia.

Alipokutana na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, walijadili hali ya Maziwa Makuu na kuipongeza Uganda kwa ujasiri na kujitolea kwake askari katika jeshi la Afrika linalolinda amani huko Somalia, AMISOM.

Bwana Ban pia alikuwa na mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amapo wawili hao walijadili hali ya Zimbwabwe na Madagascar kwa kuzingatia Tanzania ni mwenyekiti wa Troika ya SADC.

Halikadhalika Bwana Ban alikuwa na mazungumzo na Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia ambapo pamoja na kupongeza hatua zilizofikiwa alionyesha wasiwasi wake juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu hasa ukatili dhidi ya wanawake.