Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asisitiza haja ya bara la Afrika kuwajibika kwa siku zake zijazo

Ban asisitiza haja ya bara la Afrika kuwajibika kwa siku zake zijazo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema bara la Afrika lina uzoefu wa kulitosheleza kupata suluhu kwa changamoto zake, pamoja na kuchangia malengo ya kimataifa ya ukuaji unaowahusisha wote, haki ya kijamii na kulinda mazingira. Bwana Ban amesema hayo katika hotuba yake kwa viongozi wa Afrika, wakati wa mkutano wa kila mwaka wa Muungano wa Afrika kwenye makao yake mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Bwana Ban amesema baadhi ya chumi zinazokuwa kwa kasi zaidi duniani zinapatikana barani Afrika. Ameongeza kuwa mataifa mengi barani Afrika yamepiga hatua muhimu katika kuyafikia malengo ya maendeleo ya milenia; na sasa watoto wengi zaidi wa Afrika wapo shuleni, hususan wasichana, na kwamba idadi ya vifo vya akina mama wazazi imepungua, huku wanawake wengi zaidi wakihusishwa katika nafasi za kufanya maamuzi muhimu.

Bwana Ban amesema kuwa anakaribisha hatua hizo zilizopigwa, lakini bado anasikitishwa na mamilioni ya watu wa Afrika ambao wanaishi katika umaskini.

“Ufanisi utategemea uwajibikaji wa serikali na umma. Lengo letu ni dhahiri: kufikia siku za usoni ambapo rasilmali za Afrika zinawapa utajiri watu wote wa Afrika. Ambapo uongozi mbaya unapatikana tu katika vitabu vya historia. Ambapo bidhaa za Afrika zinauzwa kwa bei nzuri katika soko la kimataifa, na ambapo ushirikiano wa kimataifa unamaanisha kugawana utajiri.”

Bwana Ban amesema nchi nyingi katika bara la Afrika zilikuwa kiuchumi kwa zaidi ya asilimia 5 katika mwongo uliopita, lakini si vyema utajiri huo kusalia katika mikono ya watu wachache, kwani hali hiyo ni chanzo cha migogoro.

Amesema ni lazima kuwekeza katika vijana wa Afrika, pamoja na kuzingatia wasichana na wanawake kwa njia maalum, kwani wanaweza kuongoza harakati za amani na maendeleo.