UNHCR yaiomba Kenya ifikirie upya uhamishaji wa wakimbizi kutoka mijini

25 Januari 2013

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa limekuwa kwenye mazungumzo na serikali ya Kenya tangu mwezi Disemba baada ya serikali ya Kenya kutangaza kusitisha shughuli ya kuwapokea na kuwaandikisha watafuta hifadhi mjini Nairobi na miji mingine nchini Kenya ikisema kuwa watu hao watapelekwa kwenye kambi za wakimbizi.

UNHCR ilielezea wasi wasi wake kutokana na athari zitakazosababishwa na hatua hiyo zikiwemo usalama na haki za binadamu kwa watafuta hifadhi na pia kwenya masuala ya elimu na tegemeo la maisha la maelfu ya wakimbizi amabo wamekuwa wakiishi kihalali mijini kwa muda mrefu. UNHCR kwa sasa inaitaka serikali ya Kenya isitekeleze hatua hiyo ombi lililotupiliwa mbali na serikali . Melisa Fleming ni nmsemaji wa UNHCR.

Kambi Daadab na ile ya Kakuma zimefurika wakimbizi hakuna nafasi kabisa ya wakimbizi wengine na kwa sasa hakujakuwepo na uondokaji wa dhati kutoka kambi hizo kurejea Somalia. Hii ni kwa sababu bado hali Somalia haijatulia vizuri. Na sisi bado tuna msimamo kwamba bado ni mapema mno kuwataka wakimbizi hao warejee Somalia.

Kwa sasa kuna watafuta hifadhi na wakimbizi 56,000 walioajiandikisha na UNHCR kwenye mji mkuu wa Kenya Nairobi na miji mingine midogo nchini humo.