Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi wa Ban huko CAR azungumzia azimio la Baraza la Usalama.

Mwakilishi wa Ban huko CAR azungumzia azimio la Baraza la Usalama.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Margaret Vogt amezungumza na waandishi wa habari kwa nchi ya video kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Bangui na kusifu azimio la Baraza la Usalama ambalo amesema linasisitiza umuhimu wa ofisi yake kutoa usaidizi wa utekelezaji wa makubaliano ya Libreville.

Bi. Voght  ambaye pia anaongoza ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuimarisha ulinzi wa amani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, BINUCA amesifu pia kasi ambayo kwayo nchi kwenye ukanda huo imekuwa nayo ya kupeleka askari ili kusaidia kurejesha utulivu nchini humo.

Amesema kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kuunda kamati ya kufuatilia utekekelezaji wa makubaliano ya Libreville lakini akasema inakuwa vigumu kusimamia makubaliano wakati ambapo pia kuna matukio ya ghasia yanaendelea kutokea.

Mwakilishi huyo maalum wa Katibu Mkuu amesema huu sasa ni wakati kwa Jumuiya ya kimataifa kujihusisha kwa dhati katika kutatua mgogoro huo kidiplomasia na kutoa usaidizi wa kifedha ili kuepusha Jamhuri ya Afrika ya Kati kutumbukia kwenye matatizo zaidi.