Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laongeza muda wa ofisi yake huko CAR

Baraza la Usalama laongeza muda wa ofisi yake huko CAR

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza muda wa ofisi yake ya ulinzi wa amani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, BINUCA huku ikitaka serikali na vikundi vya upinzani kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na mengineyo yenye lengo la kurejesha amani nchini humo.

BINUCA imeongezewa muda hadi tarehe 31 mwezi Januari mwakani ambapo kupitia azimio namba 208 imetakiwa kufanya kazi  na pande zote ili makubaliano yaliyofikiwa huko Libreville Gabon tarehe 11 mwezi huu yanatekelezwa, makubaliano ambayo pia yanahusisha kuwajumuisha katika vikosi halali wapiganaji waliokuwa waasi.

Halikadhalika Baraza la Usalama limepongeza uteuzi wa mwakilishi wa upande wa upinzani ambaye atakuwa Waziri Mkuu kwenye serikali ya Umoja wa kitaifa nchini humo.

Hata hivyo Baraza limeonyesha wasiwasi juu ya usalama huko Jamhuri ya Afrika ya Kati na kutaka nchi zote na mashirika ya kikanda kusaidia kuendeleza amani kwa ushirikiano na serikali ya nchi hiyo.