Mfuko wa ufadhili wa Marekani kwa UNICEF watoa ombi la msaada kwa watoto wa Syria

24 Januari 2013

Mfuko wa ufadhili wa serikali ya Marekani kwa Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF, umetoa ombi la msaada wa dharura kwa watoto wa Syria, ambao wameathiriwa na mapigano na msimu wa baridi.

Ripoti za hivi karibuni zimeelezea jinsi watoto wa Syria wanavyoathirika zaidi na mzozo huo. Miongoni mwa takriban watu milioni mbili waliolazimika kuhama makwao nchini Syria, na laki sita na ishirini elfu ambao wamekimbilia nchi jirani, nusu yao wanakadiriwa kuwa watoto.

Ombi hilo la mfuko wa Marekani wa ufadhili linatumia picha na maandishi kuwasihi watu kulisaidia shirika la UNICEF kuhakikisha watoto wanabaki salama na kuwalinda kutokana na baridi na njaa.

Shirika la UNICEF limetoa ombi la dola milioni 68.5 kwa ajili ya misaada kwa watoto wa Syria katika kipindi cha miezi sita ya kwanza, mwaka huu wa 2013.