MONUSCO yasifu uamuzi wa Rwanda kukubali matumizi ya ndege zisizo na rubani

23 Januari 2013

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo DRC (MONUSCO) umepongeza uamuzi wa Rwanda wa kuungana na Uganda na DRC juu ya matumizi ya ndege zisizo na rubani mpakani mwa nchi hizo tatu.

Msemaji wa MONUSCO, Madnodje Mounoubai amesema kufuatia makubaliano hayo anatumai kutakuwepo na maendeleo. Amesema mapendekezo ya kutumia ndege hizo mipakani mwa DRC, Rwanda na Uganda yalitolewa na UM miaka mitano iliyopita. Hata hivyo, Bwana Mounoubai amesisitiza kuwa ni wajibu wa MONUSCO kufanya maamuzi kuhusu jinsi ya kutumia ndege hizo.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu operesheni za ulinzi wa amani Hervé Ladsous, Jumatatu 8 January, alisema kuwa MONUSCO imekuwa ikijitayarisha kutuma ndege tatu zisizo na rubani kwa ajili ya kulinda mashariki mwa DRC, suala ambalo limeungwa mkono na Ufaransa, Marekani, Uingereza na hata serekali ya DRC. Hata hivyo Rwanda ilikuwa ikipinga kwa madai kuwa ni mapema mno kufanya hivyo.