Sekta ya Kilimo Syria taabani: UM

23 Januari 2013

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliokwenda Syria kujionea hali halisi umeeleza kuwa mapigano yanayoendelea nchini humo yameathiri uzalishaji wa kilimo na hivyo msaada zaidi unahitajika maeneo ya vijijini.

Miongoni mwa waliokuwemo kwenye ujumbe huo ni Mkurugenzi wa idara ya dharura na ukarabati kutoka shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Dominique Burgeon ambaye amesema miezi 22 ya mzozo wa Syria umeporosha sekta ya kilimo ya nchi hiyo ambapo uzalishaji wa nafaka, matunda na mboga za majani umepungua kwa asilimia hamsini katika baadhi ya maeneo.

Mwingine alikuwa ni John Ging, mkuu wa operesheni wa OCHA, ambaye ameelezea hali ya kibinadamu kwa jumla

(SAUTI YA JOHN GING)

"Tumejionea moja kwa moja hatma ya watu wa Syria. Inatisha. Na ni kile ungetarajia baada ya miaka miwili ya kuzozana bila kikomo. Wengi wamekufa, wengi wamejeruhiwa, na maisha ya wengi yameharibiwa. Athari ya kisaikolojia kwa watoto ni kubwa, na ukosefu wa elimu. Tayari tunajua kwamba athari za mzozo huu zitakuwa za kudumu muda mrefu.