Hali ya chakula Myanmar shwari isipokuwa maeneo yaliyokumbwa na mikasa

23 Januari 2013

Umoja wa Mataifa unasema kuwa hali ya chakula nchini Myanmar imeimarika isipokuwa katika maeneo yaliyokumbwa na madhila ya mafuriko na mapigano ya kikabila mwaka jana.

Jarida la taarifa za hali ya kibinadamu linasema kuwa maeneo hayo ya Rakhine, Kachin na Shan Kaskazini yana maelfu ya watu waliopoteza makazi kutokana na madhila hayo mwezi Juni na Agosti mwaka 2012.

Hata hivyo jarida hilo linasema kwa ujumla kulikuwa na mazingira bora wakati wa msimu wa kupanda mazao mwezi uliopita na kwamba hali hiyo itaendelea kwa msimu wa kupanda nafaka wa mwaka 2012/2013

Limesema pia bei ya jumla ya mchele ambao ni chakula kikuu cha Myanmar imeshuka kwa miezi mitatu mfululizo tangu mwezi Oktoba baada ya kuongezeka ghafla wakati wa vurugu na mafuriko.