Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza lapitisha azimio dhidi ya DPRK, Ban aunga mkono

Baraza lapitisha azimio dhidi ya DPRK, Ban aunga mkono

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limepitisha azimio la kushutumu vikali kitendo cha Jamhuri ya kidemokrasia yaWatu wa Korea, DPRK cha kurusha roketi kwa kutumia teknolojia ya makombora ya masafa marefu mwezi Disemba mwaka jana.

Azimio hilo namba 2087 limepitishwa Jumanne baada ya mjadala wa wazi ambapo wajumbe wote wamesisitiza msimamo thabiti kuwa mpango wowote wa nyuklia wa DPRK haukubaliki.

Kufuatia hatua hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amepongeza hatua hiyo na kuitaka nchi hiyo kuzingatia maazimio yote huku akiitaka ijizuie kuchukua hatua zozote ikiwemo majaribio la nyuklia ambayo yanaweza kuongeza mvutano kwenye rasi ya Korea.

Bwana Ban amesema yeye bado anaamini kuwa mashauriano ndio njia pekee ya kuondoa nyuklia kwenye eneo hilo pamoja na kuleta amani ya kudumu.