Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utupaji chakula umekithiri: UM

Utupaji chakula umekithiri: UM

Shirika la chakula na Kilimo duniani, FAO na lile la mazingira, UNEP kwa kushirikiana na wadau wao wamezindua kampeni ya kuokoa maelfu ya Tani za chakula kinachopotea na kusababisha hasara ya dola Trilioni Moja, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutokomeza njaa duniani.

Kampeni hiyo inaitwa THINK, EAT, SAVE REDUCE YOUR FOODPRINT ambapo mashirika hayo yamesema tani Bilioni Moja nukta Tatu za chakula hupotea katika hatua mbalimbali kuanzia kinapozalishwa hadi kinapoliwa na hivyo kukwamisha harakati za kuwa na uhakika wa chakula duniani.

Wataaamu wa mashirika hayo wametaja bayana tabia ya kutupa chakula katika nchi zilizoendelea ambayo wamesema inapoteza rasilimali zilizotumika kuzalisha chakula hicho. Ann Tutwiler,ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO.

(SAUTI YA ANN )

Katika nchi tajiri, nchi zenye viwanda, karibu nusu ya chakula kinachotupwa kinaweza kutambuliwa kuwa ni mabaki ya chakula. Karibu nusu ya chakula hicho kinapotea kwa sababu wazalishaji, wauzaji wa reja reja na walaji wanatupa chakula ambacho hata hivyo bado kinafaa kuwa mlo. Iwapo utachukua chakula chote kinachotupwa katika nchi tajiri ni sawa na jumla ya chakula kinachozalishwa barani Afrika.”