Ofisi ya Haki za binadamu imesikitishwa na kunyongwa kwa kijana nchini Iran

22 Januari 2013

Kamishna ya Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu imesema kuwa umevunjwa moyo kutokana na ripoti za kunyongwa kwa kijana mmoja wa Ki-iran, aliyenyongwa January 16 mwaka huu baada ya kupatikana na hatia.

Kijana huyo Ali Naderi alitiwa hatiana na kuamuliwa kunyongwa hadi kufa kutokana na kosa alilolitenda wakati akiwa na umri wa miaka 17. Taarifa zaidi na George Njogopa.

(SAUTI YA GEORGE NJOGOPA)

Msemaji wa kamishna hiyo ya haki za binadamu Rupert Colville amesema kuwa kijana huyo aliyenyongwa akiwa na umri wa miaka 21, alikumbwa na adhabu hiyo kutokana na kukutiana na hatia ya mauwaji ya mama mmoja aliyoyafanya wakati akiwa na umri wa miaka 17.

Ameelaani utekelezwaji wa hukumu hiyo ambayo amesema imekwenda kinyume na sheria za kimataifa zinazopinga kutotumika kwa adhabu ya kifo kwa mtu ambaye alifanya kosa wakati akiwa ana umri wa chini ya miaka 18.

Adhabu hiyo pia inaelezwa kukiukwa kwa mtataba wa kimataifa juu ya haki za watoto na ule unaoangazia haki za kimsingi za kisiasa ambazo zote zinapinga utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa watoto.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameendelea kuitolea mwito Iran kukomesha adhabu ya kifo na imetaka kuwepo mashirikiana ili kuboresha ustawi wa haki za binadamu

Kiasi cha zaidi ya 400 walinyongwa katika kipindi cha mwaka jana pekee na wengi wao ni wale waliokutwa na makosa ya matumizi ya madawa ya kulevya.