Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Mali wakumbwa na uhaba wa chakula: UNHCR

Wakimbizi wa Mali wakumbwa na uhaba wa chakula: UNHCR

Wakati mashambulizi ya angani na mapigano yanapoendelea nchini Mali, wakimbizi nao wanazidi kuvuka mipaka na kuingia nchi jirani.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linasema kuwa Mauritania imepokea wakimbizi 4,208 kutoka Mali tangu tarehe 11 mwezi huu ambao kwa sasa wanahamishwa kwenda kambi ya wakimbizi ya Mbera ambayo tayari inawahifadhi wakimbizi 55,221.

Nayo Niger ina wakimbizi 1300 wapya huku Burkina Faso ikipokea wakimbizi wapya 829.

Kwa sasa UNHCR pamoja na washirika wake wanaendelea na jitihada za kuwasaidia wakimbizi walio kambini kwa kuwapa maji safi, usafi , chakula pamoja na huduma za afya na elimu.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR.

“Wale wanaowasili wametaja ukosefu wa chahkula na mafuta na kushindwa kuwepo kwa masoko. Ukosefu wa nafaka umewalazimu wafugaji wengine kuchinja mifugo yao kwa kuwa hawana chakula kingine au wanajaribu kuwauza.”

Wakati huo huo Bwana Edwards amesema UNHCR inaanzisha kambi mpya ya wakimbizi kwenye jimbo la Unity nchini Sudan Kusini ambayo itakuwa na uwezo wa kuwahifadhi wakimbizi 20,000.

Amesema UNHCR na serikali ya Sudan Kusini wamekubaliana kuweka kambi hiyo eneo la Ajuong ena wamehakikishiwa kuwa ni salama.