Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa sifa zinazotakiwa wakosesha wengi ajira: ILO

Ukosefu wa sifa zinazotakiwa wakosesha wengi ajira: ILO

Ripoti mpya ya shirika la kazi duniani, ILO kuhusu mwelekeo wa ajira inaonyesha kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na ajira duniani mwaka jana licha ya kupungua miaka miwili iliyotangulia.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Rider akizindua ripoti hiyo huko Geneva, Uswisi amesema mwaka jana kulikuwepo na watu wapya Milioni Nne nukta Mbili wasio na ajira duniani na kufanya idadi kuwa Milioni 197, ambapo robo yao hao wanatoka nchi zilizoendelea. Amesema robo tatu iliyobakia ya wasio na ajira wametapakaa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, Asia Mashariki na Asia Kusini.

Bwana Ryder amesema idadi ya watu wasio na ajira mwaka huu inatarajiwa kuongezeka kwa Milioni Mbili nukta Tatu ambapo amesema uhaba wa ajira umetokana na sababu kadhaa ikiwemo watafuta ajira kukosa stadi zinazotakiwa.

(Sauti ya Guy Rider)

Halikadhalika amezungumzia hofu iliyoghubika ILO kuhusu vijana ambapo amesema vijana wanapoteza muda mwingi bila kupata ajira na hivyo kusababisha hata kusahau stadi zao na kushindwa kupata uzoefu wa kazi.