Operesheni za ulinzi wa amani kuimarishwa: Ban

21 Januari 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu operesheni za kulinda amani za Umoja huo kwenye maeneo mbali mbali duniani ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema watakuwa wanafanya tathmini ya operesheni hizo ili kuhakikisha zina uwezo na stadi za kuwezesha kustahimili mazingira yanayoibuka wakati wa utendaji wao.

Katika hotuba yake kwa Baraza hilo Bwana Ban amesema idara ya operesheni za ulinzi wa amani na ile ya usaidizi kwenye maeneo ya kikazi zinashirikiana kuimarisha mipango ya umoja wa mataifa, usimamizi na usaidizi wa vikundi vinavyolinda amani.

(SAUTI BAN)

Tunaimarisha pia vile tunavyokuwa kwenye kipindi cha mpito wakati vikundi vya ulinzi wa amani vinapokuwa vinahitimisha kazi zao kama tulivyofanya hivi karibuni huko Timor Letse. Tunalenga kupeleka, kufanya kazi na kutimiza mamlaka tunayokuuwa tumepatiwa na kuacha misingi bora ya kujenga amani ya kudumu. Lakini tunapaswa kuongeza juhudi siyo tu ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa bali pia kuratibu washirika wetu wa kimataifa. Na kwa kiasi kikubwa mashirika ya kikanda, benki ya dunia, wahisani na nchi kwenye eneo husika kwani nazo zina nafasi kubwa.”