Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama wasilisha suala la Syria ICC: Pillay

Baraza la Usalama wasilisha suala la Syria ICC: Pillay

Kamishna Mkuu wa Tume ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay kwa mara nyingine tena amelitaka Baraza la Usalama la Umoja huo kuwasilisha suala la Syria kwenye mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC huko The Hague kwa uchunguzi.

Bi. Pillay amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani baada ya kulipatia baraza hilo muhtasari wa hali halisi ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Syria kwa kipindi cha kuanzia mwezi Agosti mwaka jana hadi Januari mwaka huu.

Bi. Pillay anasema kwamba wastani wa mauaji kwa mwezi umeongezeka kwa kiasi kikubwa ambapo awali ilikuwa Elfu moja kwa mwezi na sasa ni Elfu tano. Nimeliomba Baraza la Usalama kuwasilisha suala la Syria kwenye mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ili kuchunguza uhalifu wa kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa pande zote zinazohusika kwenye mgogoro huo.

Bi. Pillay amesema ataendelea na wito huo kwa suala hilo kuwasilishwa ICC kwa kuwa Umoja wa Mataifa hauungi mkono ukwepaji wa mkono wa sheria.

Wakati huo huo Rais wa Baraza la Usalama Balozi Masood Khan amesema wiki ijayo mjumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za kiarabu kwenye mgogoro wa Syria, Lakhdar Brahimi tarehe 29 atalipatia baraza hilo muhtasari kuhusu maendeleo ya mazungumzo ya pande tatu kwa lengo la kusuluhisha mgogoro wa Syria.