Mahiga alaani mauaji ya mwandishi habari mjini Mogadishu

18 Januari 2013

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Balozi Augustine Mahiga amelaani mauaji ya mwandishi wa habari wa Radio Shabelle, Abdihared Osman Adan, ambaye alipigwa risasi na kuuawa na wanamgambo wasiojulikana mapema hii leo mjini Mogadishu.

Huku akisema mauaji hayo ni moja ya mfululizo wa mauaji yanayolenga waandishi wa habari, Balozi Mahiga ametoa wito kwa serikali ya Somalia kuharakisha uanzishwaji wa kikosi kazi kilichotangazwa na Rais Sheikh Hassan mwezi Novemba mwaka jana kwa ajili ya kuchunguza mauaji ya waandishi habari na kuhakikisha wahusika wanapelekwa mbele ya mkono wa sheria.

Amesema vyombo vya habari vilivyo na uhuru wa kufanya kazi yao ni muhimu kwa taifa lenye demokrasia na jamii yenye usawa na kuongeza kuwa kila shambulio na vurugu dhidi ya vyombo vya habari ni mashambulizi dhidi ya utawala wa uwazi.

Halikadhalika Balozi Mahigia ametuma salaam za rambirambi kwa familia na marafiki ya Abdihared Osman na pia kwa mtandao wa habari wa Shabelle na jamii ya waandishi habari nchini Somalia kufuatia kifo hicho.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter