Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vitendo vya ubakaji huko Mali sasa ni waziwazi: UM

Vitendo vya ubakaji huko Mali sasa ni waziwazi: UM

Kamishna Mkuu wa Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Mali sasa ni dhahiri akitaja mauaji, ubakaji na mateso.

Amesema vitendo hivyo vimeelezwa kwenye ripoti ya uchunguzi itakayowasilishwa kwa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, kufuatia uchunguzi uliofanywa na wataalamu mbali mbali nchini Mali, Burkina Faso, Mauritania na Niger mwezi Novemba mwaka uliopita.

Ripoti hiyo inadhihirisha ukiukaji wa haki za binadamu umefanyika kwenye maeneo ya kaskazini na yale yaliyo chini ya udhibiti wa serikali. Rupert Colville ni msemaji wa tume ya haki za binadamu.

(SAUTI RUPERT COLVILLE)

Ubakaji wa wanawake na wasichana , wakati mwingine mbele ya familia zao na unaofanywa ukilenga makabila umekuwa ukitumika kila mara kaskazini ili kuwanyanyasa na kujenga hofu jamii kwenye tamaduni ambapo ubakaji unachukuliwa kuwa mwiko na waathiriwa kutengwa na jamii. Wasichana wadogo wakati mwingine wenye umri wa miaka 12 au 13 wanaripotiwa kuozwa kwa lazima kwa wafuasi wa Ansar Dine, MUJAO na AQMI(Al-Qaida au Maghreb islamique) na kubakwa kwa siku kadhaa.