Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola Milioni 30.5 zahitajika kuwatia nuru wakazi wa Kivu Kaskazini

Dola Milioni 30.5 zahitajika kuwatia nuru wakazi wa Kivu Kaskazini

Umoja wa Mataifa na washirka wake wa utoaji wa misaada unaomba dola Milioni 30 na Nusu kwa ajiliya watu Elfu 59 walioathirika na mapigano ya hivi karibuni kwenye jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi

(SAUTI YA ASSUMPTA MASSOI)

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu, OCHA huko DRC, Barbara Shenstone amesema mpango wa miezi Sita wa usaidizi huko Kivu Kaskazini ni jibu la matatizo na mateso yaliyowakumba maelfu ya watu kwenye eneo hilo miezi ya karibuni.

Amesema fedha hizo zitawezesha familia husika kupatiwa mahitaji muhimu kama vile mablanketi, maji safi na salama wakati OCHA ikitafakari jinsi ya kurejesha maisha yao ya kawaida.

OCHA inasema kuwa licha ya mapigano kutokuwepo kwa sasa huko Kivu Kaskazini, bado kuna hali ya wasiwasi kutokana na kuzagaa kwa silaha na mapigano ya hapa na pale kati ya vikundi vyenye silaha.

Mpango huo wa miezi sita ni sehemu ya mpango wa usaidizi kwa DRC wenye thamani ya dola Milioni 892 utakaozinduliwa wiki chache zijazo mjini Kinshasa.