Kazi bado kubwa kudhibiti vifo vya wajawazito

17 Januari 2013

Mkutano wa kimataifa kuhusu afya ya wajawazito umemalizika huko Arusha Tanzania ambako imeelezwa kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana kupunguza vifo vya wajawazito, bado kuna changamoto ili kuweza kufikia lengo la Milenia la kupunguza vifo hivyo kwa asilimia 75.

Katika mahojiano maalum na Radio ya Umoja wa Mataifa, Naibu Waziri wa afya wa Tanzania Dkt. Seif Rashid ametaja changamoto hizo kuwa ni upatikanaji na ufikiaji wa huduma za afya pamoja na huduma mbovo kwa wajawazito.

Hata hivyo amesema washiriki wakiwemo watunga sera, wataalamu na wanaharakati walibadilishana njia bora za kurekebisha mwelekeo huo.

(SAUTI YA DKT. RASHID)

Kuhusu ripoti kuwa vifo vya wajawazito ni vingi mijini kuliko vijijini Naibu Waziri huyo wa afya amesema sababu ni uwezo mdogo wa kupata usafiri kwa wakati, idadi kubwa ya wakazi wa mijini, uhaba wa wodi za wazazi na ukosefu wa utangamano wa kusaidiana haraka kama ilivyo vijijini.