Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uamuzi wa Rais Rajoelina ni wa busara: Ban

Uamuzi wa Rais Rajoelina ni wa busara: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesifu uamuzi wa Rais wa mpito wa Madagascar Andry Rajoelina, wa kutogombea wadhifa huo katika kinyang’anyiro cha Urais mwezi Mei mwaka huu.

Bwana Ban amekaririwa akisema kuwa kitendo cha Rais Rajoelina pamoja na ahadi ya awali ya Rais wa zamani Marc Ravalomanana, vitasaidia kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki na hatimaye kumaliza kipindi cha mpito.

Halikadhalika amesema itakuwa vyema Madagascar ikazingatia kalenda ya uchaguzi wake iliyoridhiwa na tume huru ya mpito ya uchaguzi.

Bwana Ban amesema pia ni vyema mpango wa mwaka 2011 wa kumaliza mgogoro nchini Madagascar hususan vipengele vinavyohusu mikakati ya kujenga imani, vikatekelezwa ipasavyo.

Katibu Mkuu huyo amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake uko tayari kuendelea kusaidia serikali na wananchi wa Madagascar.