Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamateni wabakaji na si waandishi: Bangura

Kamateni wabakaji na si waandishi: Bangura

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya ukatili wa kingono katika maeneo ya migogoro, Hawa Zainab Bangura amezungumzia sakata la kushikiliwa kwa mwandishi wa habari nchini Somalia baada ya kumhoji mwanamke anayedaiwa kubakwa na askari wa jeshi la nchi hiyo ambapo ametaka serikali kumwachia mara moja mwandishi huyo.

Katika taarifa yake Bi. Bangura amesema tuhuma za ubakaji zinapaswa kuchunguzwa kwa kina badala ya kuwatia nguvuni wahanga wa tukio hilo au waandishi wa habari wanaoripoti uhalifu wa aina hiyo.

Amesema hatua iliyochukuliwa na polisi wa Somalia kumkamata mwandishi wa habari ni kinyume na haki na kinamtia hatiani zaidi mhanga wa tukio hilo na kubinya uhuru wa kujieleza kupitia vyombo vya habari.

Bi. Bangura amesema wahanga wa ubakaji hawapaswi kuishi kwa hofu huku watuhumiwa wakilindwa na wakiishi huru na hivyo ametaka polisi kukamata wabakaji na siyo waandishi wa habari.

Inadaiwa kuwa mwanamke husika alibakwa na askari wa jeshi la Somalia mwezi Septemba mwaka jana ambapo waandishi wa habari waliomhoji walikamatwa pamoja na mwanamke husika.