Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nafuatilia kwa karibu hali ya Mali: Ban

Nafuatilia kwa karibu hali ya Mali: Ban

Wakati  hali ya usalama ikiripotiwa kuendelea kuzorota huko Mali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema anafuatilia kwa karibu hali hiyo ambapo tayari amezungumza na Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, Rais Alassane Ouattara wa Côte d'Ivoire .

Bwana Ban amekaririwa na msemaji wake akieleza kujulishwa juu ya mkutano wa ECOWAS utakaofanyika tarehe 19 mwezi huu pamoja na mpango wa nchi wanachama kupeleka askari wao huko Mali.

Tayari Bwana Ban amezungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Laurent Fabius ambaye pia amemjulisha operesheni za kijeshi zinazoendeshwa na Ufaransa nchini Mali kufuatia ombi la dharura la nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Katibu Mkuu ameunga mkono vile washirika wa Mali wanavyochukua hatua kwa ridhaa ya nchi hiyo ya kutaka msaada ili kukabiliana na vikundi vyenye silaha vinavyoendelea kusonga kusini mwa nchi hiyo.

Bwana Ban amesema hatua za sasa zinaongeza umuhimu wa kutekeleza haraka azimio 2085 la Baraza la usalama la kutaka kurejeshwa kwa utawala wa kikatiba nchini Mali.

Halikadhalika amesema maandalizi yanaendelea kupeleka jopo la wataalamu mbali mbali huko Bamako Mali watakaofanya kazi kwa pamoja na serikali kuharakisha mchakato wa kisiasa na kiulinzi.