Jeshi la kimataifa kuungana na MONUSCO: Gaye

14 Januari 2013

Mshauri wa masuala ya kijeshi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jenerali Babacar Gaye, amesema kuunganishwa kwa jeshi la kimataifa linalokwenda mpakani wa Rwanda na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, DRCna kikosi cha MONUSCO kutasaidia kupunguza gharama za fedha.

Jenerali Gaye amesema hayo alipozungumza na Radio Okapi baada ya kurejea kutoka Addis Ababa, Ethiopia ambako alihudhuria mkutano wa mawaziri na wakuu wa nchi za Maziwa Makuu kuhusu kupelekwa kwa kikosi hicho.

(SAUTI YA BABACAR GAYE)

Umoja wa Mataifa unatoa ufumbuzi kwa matatizo matatu. Kwanza ni suluhisho la tatizo la kugharimu kikosi hicho kwa sababu sasa kitakuwa sehemu ya MONUSCO. Pia tunachangia katika kusuluhisha tatizo la ghasia inayoendelea mashariki mwa DRC. Kikoshi hicho kitakuwa chini ya walinda amani wa UM.

Amesema brigedi hiyo itakuwa ni mpya ndani ya MONUSCO ambayo tayari ina brigeti tatu katika Kivu ya Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.

(SAUTI YA BABACAR GAYE)

Brigedi hiyo itakuwa kamilifu ndani ya sehemu ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Hivyo brigedi hiyo itakuwa chini ya amri ya kamanda wa nne na itatekeleza wajibu wake chini ya mamlaka ya mwakilishi maalum wa UM.

Jenerali Gaye alisema kuwa Umoja wa Mataifa utazitaka nchi za ukanda huo kuchangia askari kwa kikosi hicho.