Chuki za kidini hazina nafasi karne ya 21: Ban

12 Januari 2013

Chuki inayojengwa kwa misingi ya imani ya dini haina nafasi karne hii ya 21 ambayo tunaendelea kuijenga. Na hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliyoitoa leo mjini New York, Marekani wakati wa kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya wayahudi yaliyotekelezwa na serikali ya Adolf Hitler.

Bwana Ban amesema wakati wa mauaji hayo, mtu yeyote aliyekwenda kinyume na msimamo wa Hitler, kama vile myahudi, mroma, msinti, shoga au mkomunisti alikamatwa na kupelekwa kwenye kambi za mateso akisubiri kuuawa.

Amesema misingi ya chuki inabomoa na akasema ndio maana ana hofu na mkwamo wa mazungumzo kati ya Palestina na Israeli na hivyo ni vyema misingi ya chuki ikawa haina nafasi na vijana wakakuzwa katika mazingira ya kuvumiliana na kuishi kwa pamoja.

Halikadhalika ametumia fursa hiyo kugusia Syria na kueleza kuchelewa kuwa kutatuliwa kwa mgogoro huo kutasababisha upanuke na kusambaa kwa misingi ya kidini au kikabila.

Amerejelea wito wake wa kulitaka Baraza la Usalama kufanya uamuzi wa dhati kushughulikia mgogoro huo ambao amesema unakua siku hadi siku.