Mzozo CAR, Baraza la usalama lasifu makubaliano ya Libreville

12 Januari 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesifu mashauriano yaliyofanyika huko Libreville Gabon, na kuwezesha kutiwa saini kwa makubaliano ya kimsingi ya kusitisha mapigano na kupatia suluhu la kisiasa mzozo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Taarifa ya  Baraza hilo iliyotolewa mwishoni mwa kikao maalum kuhusu hali ya usalama nchini humo imesema wajumbe wanataka kuharakishwa kwa utekelezaji wa makubaliano hayo na pande zote husika kufanya hivyo kwa nia njema ili amani ya kudumu iweze kupatikana.

Halikadhalika Baraza limesifu jitihada za Umoja wa Afrika na taasisi za kikanda za kusuluhisha mgogoro huo na kuelezea kuunga mkono juhudi za mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja  wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Margaret Vogt.

Hata hivyo Baraza limeeleza kusikitishwa kwake na ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo mashambulizi yanayolenga makundi madogo na ukatili wa kingono na kutaka vitendo hivyo viachwe mara moja na wahusika wawajibishwe.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter