Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lahitajika jeshi thabiti CAR: Vogt

Lahitajika jeshi thabiti CAR: Vogt

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo limeelezwa jinsi hali  ya usalama ilivyo tete huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako jeshi linashindwa kudhibiti waasi wanaoendelea kushikilia miji kadhaa nchini humo.

Taarifa hizo zimetolewa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu waUmoja wa Mataifa nchini humo Margaret Voght wakati akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu hali halisi Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa njia ya video kutoka Libreville, Gabon.

Bi. Vogt amesema hali nchini humo ilikuwa ilitengamaa kwa kiasi na kuonyesha matumaini ya ujenzi wa miundombini ya amani, ulinzi, usalama , uchumi na kijamii kama vile IMF kukubali kuondoa vikwazo vya nchi hiyo kupata fedha kutoka nje na kupata misaada ya kigeni iliyokuwa imezuiliwa kwa miaka mitatu.

Hata hivyo Bi. Vogt ambaye anasimamia pia ofisi ya Umoja wa Mataifa ya ujenzi wa nchi hiyo BINUCA amesema mambo yalibadilika ghafla na kuweka usalama wa wananchi mashakani.

“Kwa bahati mbaya mafanikio hayo yalikwamishwa na kurejea upya kwa mgogoro, baadhi ya vikundi vilianza mashambulizi kwenye miji kadhaa kaskazini mashariki. Kikundi cha waasi cha Seleka kinachojumuisha vikundi vya waasi  kimeweza kudhibiti miji kadhaa bila upinzani kutoka jeshi la serikali. Kushindwa kwa jeshi la kitaifa kuzuia waasi hao ni kiashirio cha kuporomoka kwa jeshi la ulinzi. Jeshi limepoteza mwelekeo na utayari wa kupigana, askari wengi wamesalimisha silaha zao  na wamekimbilia porini. Ndani  ya wiki chache karibu nusu ya mikoa yote ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ilichukuliwa na waasi.”

Wakati  huo huo Bi. Vogt ameiambia Radio ya Umoja wa Mataifa kuwa pande husika katika mgogoro huko Jamhuri ya Afrika ya Kati zimetiliana saini mjini Libreville makubaliano ya kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa na pia yanatoa fursa kwa vikwazo kuwekwa iwapo makubaliano  hayo yatakumbana na matatizo ya utekelezaji.