Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya Pakistani yanitia wasiwasi: Ban

Hali ya Pakistani yanitia wasiwasi: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameeleza kusikitishwa kwake na mwendelezo wa mashambulizi ya kigaidi nchini Pakistani akigusia shambulio la jana na la leo.

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya msemaji wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban ameshutumu mashambulio hayo katika eneo la Quetta na Swat ambayo yamesababisha vifo vya watu wapatao 100 na wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa. Halikadhalika ameshutumu shambulio la jana lililomlenga na kumuua Dkt Syed Riaz Hussain aliyekuwa Rais wa chama cha Pakistani People.

Bwana Ban amesema Dkt. Hussein alikuwa mtetezi wa dhati wa demokrasia na aliamini katika kuvumiliana.

Katibu Mkuu amesema matukio hayo ya kikatili hayawezi kuhalalishwa kwa misingi yoyote ile na ametuma salamu za rambi rambi kwa serikali, wananchi wa Pakistani na familia za waliokumbwa na mikasa hiyo.

Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unaunga mkono kwa dhati jitihada za serikali ya Pakistani za kupambana na ugaidi na ni matumaini  yake kuwa watekelezaji wa mashambulio hayo watafikishwa mbele ya sheria.