Ladsous aanza ziara Haiti

10 Januari 2013

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu operesheni za ulinzi wa amani Hervé Ladsous, amesema kazi iliyopo hivi sasa nchini Haiti, miaka mitatu baada ya tetemeko kubwa la ardhi ni kujikita zaidi katika kujenga jeshi la polisi la kitaifa na kuimarisha wa utawala wa kisheria.

Bwana Ladsous amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Port au Prince, nchini Haiti siku mbili kabla nchi hiyo haijafanya kumbukumbu ya miaka mitatu tangu kutokea kwa tetekemeko hilo lililosababisha vifo vya zaidi ya watu Laki Tatu wakiwemo watumishi zaidi ya 100 wa umoja wa Mataifa.

Tayari Bwana Ladsous amekuwa na mazungumzo na Rais Michel Martelly na pia anatarajiwa kukutana na maafisa kadhaa wa serikali, ikiwemo waziri wa mambo ya nje na maafisa na wafanyakazi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kurejesha utulivu Haiti, MINUSTAH.