Biashara haramu ya tumbaku sasa mtegoni: WHO

10 Januari 2013

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO, Dkt. Margaret Chan amesema itifaki mpya ya kutokomeza biashara haramu ya bidhaa zitokanazo na tumbaku inaipatia dunia fursa ya kipekee ya kudhibiti njia za kisasa za kitendo hicho cha kihalifu chenye gharama kubwa hususan kwa afya za binadamu.

Dkt.Chan amesma hayo leo mjini Geneva, Uswisi wakati wa hafla maalum ya kuanza kutiwa saini kwa itifaki hiyo iliyopitishwa wakati wa mkutano uliofanyika Seoul, Korea Kusini mwaka jana.

Amesema biashara haramu ya tumbaku inatoa fursa ya watu kupata bidhaa zitokanazo na zao hilo kwa bei nafuu na hivyo kukinzana na harakati za WHO za kupambana na uvutaji wa sigara na bidhaa zingine za tumbaku.

(SAUTI YA Dkt. CHAN)

Wawakilishi kutoka nchi 12 wanachama wa mkataba huo ikiwemo China, Ufaransa, Gabon, Libya, Myanmar, Nicaragua, Panama, Jamhuri ya Korea na Afrika Kusini walitia saini itifaki hiyo. Baada ya Geneva, shughuli ya utiaji saini itahamishiwa New York, Marekani hadi tarehe Tisa Januari mwakani na itaanza kutumika siku 90 baada ya nchi ya 40 kutia saini.