Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria zitungwe kulinda wafanyakazi wa majumbani: ILO

Sheria zitungwe kulinda wafanyakazi wa majumbani: ILO

Ripoti mpya ya shirika la kazi duniani, ILO imeweka bayana kuwa bado kazi za majumbani zinadharauliwa licha ya mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jamii. ILO inasema ajira hiyo ni ya manyanyaso, kuanzia muda wa kazi hadi maslahi. Ripoti inaonyesha kuwa kiidadi, wafanyakazi hao wanaongezeka lakini maslahi yao yanazidi kuwa duni hasa katika nchi zinazoendelea. Je nini msingi wa hali hiyo? Je Tanzania nini kinafanyika? Basi ungana na Assumpta Massoi katika ripoti hii.

Kulea watoto, kutunza wazee na hata watu wenye ulemavu, kufanya kazi mbali mbali za majumbani kama vile kupika, kufua na usafi ni baadhi tu ya majukumu yanayowakabili wafanyakazi wa majumbani sehemu mbali mbali duniani. Shirika la kazi duniani, ILO linasema kuwa sekta hii ya kufanya kazi majumbani inakua ambapo idadi imeongezeka kutoka Milioni 19 mwaka 2010 hadi Milioni 52 mwaka huu lakini bado imegubikwa na unyanyasaji wa kupindukia.

Mathalani ILO inasema kuwa wafanyakazi hawa hufanya kazi saa nyingi kupita kiasi kwa ujira mdogo, na bado jamii hasa katika nchi maskini inawadharau na hali hiyo inawafanya wawe hatarini zaidi kuteseka. Sandra Polaski ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ILO na hapa ni mjini Geneva wakati akizindua ripoti ya hali ya wafanyakazi wa majumbani.

(SAUTI YA SANDRA)

"Hii ripoti yetu ya leo imeweka bayana kuwa wafanyakazi wa majumbani ni sehemu kubwa ya nguvukazi ya dunia kuliko vile ilivyodhaniwa na mara nyingi wanatumikishwa na kunyanyaswa katika kiwango ambacho hakiwezi kuvumiliwa na wafanyakazi wa sekta zingine. Majukumu na mazingira ya kazi zao kwa muda mrefu yameenguliwa katika sera za umma, mijadala na hata utungaji sera. Ijapokuwa ni moja ya kazi za siku nyingi, sera na sheria za ajira na masuala ya kijamii katika nchi hazijazingatia watumishi wa majumbani,.”

Bi Sandra akaenda mbali zaidi na kugusia muda wa kazi.

(SAUTI Sandra)

ASSUMPTA: Naibu Mkurugenzi huyo wa ILO anasema kuwa msingi mkuu wa manyanyaso ni uhusiano wa Ubwana na Utwana kati ya mwajiri na mwajiriwa katika kazi hiyo iliyopo duniani tangu enzi na enzi ambayo pia itaendelea kuwepona hivyo muhimu ni kuinua hadhi na maslahi yake kwa kuweka sheria. Katika ripoti hiyo, Tanzania imetajwa kuwa ni nchi ambamo wastani wa saa za kazi kwa wiki kwa watumishi wa majumbani zimekithiri na kufikia saa 63 badala ya wastani wa kimataifa wa saa kati ya 40 na 48 kwa wiki. Anne-Marie Kiaga ni Mratibu wa mpango wa misaada ya maendeleo katika ofisi ya ILO nchini Tanzania, anasema kwa Tanzania sheria za kutambua wafanyakazi hao zipo lakini kuna changamoto.

(SAUTI – ANNE)

Bi. Kiaga anasema udugu unatia tatizo zaidi..

(SAUTI ANNE-MARIE)

Kwa sasa ILO kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania na mashirika yasiyo ya kiserikali inafanya utafiti wa kina kufahamu wa idadi halisi ya wafanyakazi wa majumbani nchini humo utakaokamilika mwezi huu, huku Wizara ya Kazi ikijizatiti kuelimisha umma kwa lengo la kuboresha sekta hiyo.

(SAUTI – ANNE-LAST)

Mkataba wa kimataifa wa ILO kuhusu kazi za majumbani uliopitishwa mwaka 2011 pamoja na mambo mengine unaweka viwango sawa  mathalani vya saa kazi kati ya watumishi wa majumbani na wale wa sekta nyingine. Mkataba huo utaanza kutumika rasmi mwezi Septemba mwaka huu. Mkataba huo.

Bila shaka utafiti huo utaleta majibu ya kuinua hadhi ya wafanyakazi wa majumbani. Shukrani Assumpta nami ni Monica Morara kwaheri kwa sasa.