Ban aunga mkono azma ya Abe ya kuinua uchumi wa Japan

9 Januari 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amekuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu mpya wa Japan Shinzo Abe ambapo pamoja na kumpongeza kwa wadhifa huo mpya, amesema anaunga mkono azma ya Abe ya kujenga upya uchumi wa Japan baada ya tetemeko kubwa la ardhi la mwaka 2011 pamoja na Tsunami.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amemkariri Bwana Ban akimsisitizia pia Bwana Abe kuhusu dhima ya Japan huko Kaskazini Mashariki mwa Asia na kupongeza jitihada za nchi hiyo kuhusu kuondokana na silaha za nyuklia.

Hata hivyo ameeleza wasiwasi wake kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini na hali ya haki za binadamu nchini humo na umuhimu wa kupatia suluhu suala la mateka.

Abe kwa upande wake amekubaliana na masuala yaliyoibuliwa na Bwana Ban na kuelezea azma yake ya kuimarisha uhusiano kati ya Japan na Umoja wa Mataifa na Japan na nchi jirani.