Mapigano Darfur ya kati yanaathiri raia: UNAMID

9 Januari 2013

Kaimu mjumbe maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur, UNAMID Aichatou Mindaoudou ametembelea mji mkuu wa jimbo la Darfur ya Kati, Zalingei ambapo ameelezea wasiwasi wake juu ya mapigano yanayoendelea kwenye mji wa magharibi wa Jebel Marra.

Ameelezea wasiwasi wake huo baada ya mazungumzo na gavana wa jimbo hilo Dkt. Yousif Tibin ya kwamba vikundi vyenye silaha vinadhibiti miji ya Golo na Rockero kwenye eneo hilo ambapo familia 850 hazina makazi na zingine zimekimbilia milimani.

Bi. Mindaoudou ametaka kusitishwa kwa mapigano hayo na ametaka pande katika mzozo huo kuheshimu haki za binadamu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Amemhakikishia Gavana Tibin kuwa UNAMID kwa upande wake itaendelea kusaidia uwezeshaji wa kuwapatia misaada ya kibinadamu wale wanaohitaji.

Wakati wa ziara hiyo Bi. Mindaoudou alizindua miradi mitatu ikiwemo ya madarasa na vyoo kwa ajili ya shule. Tangu mwaka 2007 UNAMID imeshakamilisha miradi ya aina hiyo ya matokeo ipatayo 500 yenye thamani ya dola Milioni 15.