Hali za wakimbizi huko Sudan ni mbaya: Ging

8 Januari 2013

Mamia ya maelfu ya watu waliopoteza makazi yao kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya majeshi ya serikali na vikundi vya waasi wenye silaha kwenye majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile nchini Sudan wanakabiliwa na hali mbaya ya maisha.

Hiyo ni kauli ya Mkurugenzi wa OPeresheni wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu, OCHA John Ging aliyoitoa mbele ya Baraza la Usalama hii leo wakati wa mashauriano ya faragha kuhusu hali iliyvo kwenye majimbo hayo.

Baadaye Bwana Ging aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuna watu Laki Tisa ambao wamepoteza makazi, wamekimbia makazi yao au wako katika mahitaji makubwa ya kibinadamu kwenye majimbo hayo mawili.

Sehemu ya tatizo letu kama Umoja wa Mataifa ni kwamba hatuwezi kufika kuwasaidia walipo na hata kubaini kwa dhahiri matatizo yao. Sisi, bila shaka tunawapokea kama wakimbizi, tunasikiliza simulizi zao, tunaona vile walivyo. Tunasikia habari za kusikitisha kutoka kwao kama vile wanavyoathirika na mgogoro unaoendelea kwa kutokuwa na chakula au msaada wa tiba ambao wanahitaji na mazingira duni ambamo wanaishi.”

 

Bwana Ging amesema kuna jitihada za Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za kiarabu za kuwezesha serikali ya Sudan na waasi kuruhusu wafanyakazi wa misaada kusambaza misaada ya kibinadamu.

Hata hivyo amesema hadi sasa jitihada hizo hazijazaa matunda na ameonya kuwa iwapo suluhisho halitapatikana wakazi wengi wa majimbo hayo ya Kordofan Kusini na Blue Nile watakufa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter